Thursday, March 5, 2020

NAFASI YA MIGUU KATIKA ULIMWENGU WA ROHO


 TAMBUA NAFASI YA MIGUU KATIKA ULIMWENGU WA ROHO. JIFUNZE KUOMBEA MIGUU NA ARDHI UNAYOISHI ILI UMSIKIE MUNGU ANAPOSEMA NAWE JUU YA MPANGO WAKE KATIKA MAISHA YAKO

 


Ukisoma biblia utaona kuna viungo ambavyo vilipewa nafasi fulani katika ulimwengu wa roho ili tuvitumie kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Baadhi ya viungo hivyo ni masikio na miguu ya mtu wa ndani. Leo tuangalie kwa upana juu ya nafasi ya miguu katika ulimwengu wa roho, uhusiano wake na nafsi, na kile mtu anaamua katika maisha.
Mungu anaepusha miguu yetu isiende katika njia mbaya ili tuweze kutii neno lake (Zaburi 119:101). Ukimtii Mungu na sheria zake katika njia zako zote atayanyosha mapito yako nawe utafanya maamuzi sahihi (Methali 3:6).
Mguu wako ukiwa msafi kwa jinsi ya rohoni unakupa kumsikia Mungu. “Jitunze mguu wako uendapo nyumbani kwa Mungu; Maana ni heri kukaribia ili usikie” (Mhubiri 5:1).
Mungu alipotaka kusema na Musa juu ya mpango wake alimwambia avue viatu kwani mahali aliposimama ni patakatifu (Kutoka 3:5). Yule amiri jeshi wa BWANA naye alimwambia Joshua kitu hiki (Joshua 5:15). Kwa hiyo Mungu alitaka miguu yao ndio ikanyage patakatifu ili aweze kusema nao.
Miguu yako ikiwa misafi kwa jinsi ya rohoni maana yake unaandaliwa kutimiza kusudi la Mungu. Yule mwanamke alipompaka marhamu Yesu katika miguu, kitendo kile kilikuwa cha kiroho na ilikuwa kuupaka mwili wa Yesu marhamu tayari kwa maziko. Na Yesu alisema tendo hili litakumbukwa popote injili ya ufalme itakapo hubiriwa (Marko 14:3—9; Luka 7:37—50).
Katika karamu ya mwisho, Yesu aliosha miguu ya wanafunzi. Petro alitaka kukataa na Yesu akamwamabia asipomuosha miguu hana ushirika naye (Yohana 13:1—8). Kwa nini aoshe miguu na siyo viungo vingine? Kwa nini neno linasema "Ni mizuri kama nini miguu yao wapelekao habari ya mema!" (Warumi 10:15). Kwa hiyo kuna ambayo nafasi miguu imepewa katika ulimwengu wa roho.
Miguu ni lango la kiroho la nafsi ya mtu. Miguu inaweza kuwa misafi au michafu kwa jinsi ya rohoni. “Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu” (Methali 6:18). Neno linatuambia tusiende njiani pamoja nao watendao maovu na tusiweke mguu wetu katika mapito yao kwani miguu yao huenda maovuni (Methali 1:15—16).
Mtu anatembea katika ubatili pale miguu inapokimbilia udanganyifu (Ayubu 31:5). Shetani akikamata miguu ya mtu amekamata nafsi yake na akikamata nafsi anazuia kusudi la Mungu katika mtu huyo.
Ndio maana Mungu akitaka kuiokoa nafsi yako anaimarisha miguu yako. “Maana umeniponya miguu yangu na mauti; Je hukuizuia miguu yangu isianguke? Ili nienende mbele za Mungu katika nuru ya walio hai” (Zaburi 56:13).
Muombe Mungu atakase miguu yako ili ishikamane na mpango alioukusudia katika maisha yako. “Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikudondoshwa” (Zaburi 17:5). Mungu akutoe katika shimo lolote la uhabirifu na asimamishe miguu yako katika mwamba na kuimarisha hatua zako zote (Zaburi 40:2). Anayesikia neno la ufalme la kulitenda analinganishwa na mtu aliyejenga nyumba juu ya mwamba (Matayo 7:24).
Adui anapokuja na kushusha nguvu zako za kiroho, Mungu hukomboa miguu au sikio (Amosi 3:11—12). Mungu anakomboa miguu au sikio ili tuweze kumsikia na kujua kusudi lake. Mungu anakulinda na adui kwa kulinda miguu yako. “Wala hukunitia mikononi mwa adui; miguu yangu umeisimamisha panapo nafasi” (Zaburi 31:8).
Kuna watu ambao wamekuwa wanaota ndoto zinazohusiana na miguu na ardhi. Kuna ambao wanaota wapo sehemu halafu wanakosa mahali pa kukanyaga au pa kuweka miguu yao.
Kuna mtu alinitumia ndoto aliyoota akiwa nyumbani kwake. Lakini sebuleni palikuwa pachafu. Mwingine akaota maji ya chooni yamemwagika chini na akajikuta anayakanyaga. Wengine wanaota wadudu, wanyama au nyoka wanauma miguu yao. Wengine wanaota miguu mizito hawawezi kukimbia au wamevaa viatu vinavyowapa shida kutembea.
Kuna watu huwa wanaota ndoto wapo sehemu yenye maji au uchafu na hamna mahali pa kukanyaga na wengine wanajikuta wamekanyaka mahali penye maji machafu, matope au sehemu ambayo kwa jinsi ya kawaida mtu huwezi kukanyaga.
Ukiota ndoto za aina hiyo, muombe Mungu akuongoze katika maamuzi ambayo unataka kuyafanya au umeyafanya. Mvua ya gharika ilipoisha baadae Nuhu alituma njiwa naye alikosa mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake hivyo akarudi kwenye safina (Mwanzo 8:8—9).
Unapotaka kufanya maamuzi ya muhimu katika maisha, amani ya Kristo iamue moyoni mwako. “Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu” (Wakolosai 3:15a). Kuna uhusiano kati ya miguu na amani kuamua ndani yako. “Kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti, Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani” (Luka 1:79).
Neno linatuambia tuvae silaha zote za Mungu kwani tunapigana na falme na mamlaka, na wakuu wa giza hili, na majeshi ya mapepo wabaya katika ulimwengu wa roho (Waefeso 6:11—12). Moja ya silaha tumepewa ni Injili ya amani. Neno linasema tufungiwe miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani” (Waefeso 6:15).
katika vita vya kiroho, amani ni silaha ya kutumia kumshinda Shetani. “Naye Mungu wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi” (Warumi 16:20a). Kama unataka kufanya jambo kinyume na Mungu utakosa amani na Roho Mtakatifu ataweka uzito wa wewe kuchukua hatua.
Shetani naye akikamata miguu ya mtu anaweka wepesi kwenda kutenda maovu (Isaya 59:7). Miguu ni kiungo adui anakiwinda kwani ni mlango wa nafsi. Zaburi 56:6 inatuambia “hukutanika, hujificha, huziangalia nyayo zangu, Kwa kuwa wameniotea nafsi yangu.” Adui wakati wote atapeleleza hatua zako. “Hunitia miguu yangu katika mkatale, Na mapito yangu yote huyapeleleza” (Ayubu 33:11).
Lakini haijalishi Shetani anafatilia maisha yako vipi, Mungu ametuahidi katika neno lake ya kwamba anaifanya miguu yetu kuwa ya kulungu (Zaburi 18:33; Habakuki 3:19). Kulungu ni mnyama ambaye miguu ya nyuma inakanyaga palepale miguu ya mbele ilipopita. Hivyo Mungu anataka tukanyage katika hatua zake.
Mungu ndiye anayeimarisha hatua zetu (Zaburi 37:23). Mungu ndiye anayeweka uhai katika nafsi zetu wala hatatuacha mguu wetu usogezwe (Zaburi 66:9). Mungu atakulinda na mabaya na kuikomboa nafsi yako (Zaburi 121:7).
Nyoka alipomdanganya mwanamke kula matunda Mungu aliyowakataza “BWANA Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umefanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino” (Mwanzo 3:14—15).
Maandiko haya yanatufundisha kuwa nyoka kutembelea tumbo ni adhabu Mungu alimpa. Kwa hiyo kabla ya dhambi nyoka hakutembelea tumbo (maandiko hayatuambii alitembeaje). Nyoka, ambaye anasimama badala ya Shetani katika ulimwengu wa roho, anawinda miguu.
Ndio sababu Yesu ametupa nguvu ya kumkanyaga nyoka. “Tazama nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru” (Luka 10:19). Mtu haweza kukanyaga nyoka kama hana mguu wa kukanyagia. Hatuwezi kumshinda Shetani ila kwa nguvu za Mungu pekee.
Baada ya anguko, ardhi ililaaniwa (Mwanzo 3:17). Ardhi ina uwezo wa kubeba maneno mtu asifanikiwe kimaisha. “Ee nchi, nchi, nchi, lisikie neno la BWANA. BWANA asema hivi, Andikeni habari za mtu huyu kwamba hana watoto, kwamba mtu huyu hatafanikiwa siku zake zote; maana hapana mtu katika wazao wake atakayefanikiwa, akiketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na kutawala katika Yuda” (Yeremia 22:29—30).
Kama ardhi imebeba laana na ina uwezo wa kubeba maneno dhidi ya mtu; na ardhi hiyo ndiyo mtu anatakiwa kuikanyaga maana yake katika ulimwengu wa roho kuna kiunganishi/uhusiano kati ya ardhi na miguu. Katika ndoto ya Nebukadneza miguu ilikuwa nusu chuma na nusu udongo (Daniel 2:32—33).
Ardhi ndio mahali pa Mungu kuweka miguu yake (Matayo 5:35; Isaya 66:1). Mungu aliwapa wana wa Israel kumiliki kila ardhi ambapo nyayo za miguu yao zitakanyaga (Kumbukumbu 11:24a). Kumbuka umiliki wa ardhi ni jambo la rohoni kwanza ndipo la kimwili. Siyo kila anayemiliki ardhi kwa jinsi ya mwili pia anamiliki katika ulimwengu wa roho.
Wana wa Israel walipewa kumiliki pale nyayo zao zitapokanyaga. Kwa hiyo siyo kila unapokanyaga unamiliki. Wakati mwingine hali yako ya kiroho inategemea nani anayemiliki katika ulimwengu wa roho eneo ulilokanyaga.
Mungu alimwambia Musa kuwa ardhi aliyokuwa amesimama ilikuwa takatifu. Kwa hiyo kuna ardhi ambayo siyo takatifu na inamilikiwa na miungu mingine. Kama miguu yako ikikanyaga
eneo hilo, uwe na uhakika nguvu zako za kiroho zitakutoka na kuna kiwango cha kuyatenda mapenzi ya Mungu ambacho utakwama.
Unaweza kupita katika njia lakini huwezi kujua nani amepita kabla yako na kwa kusudi lipi. “Maana mfalme wa Babeli alisimama penye njia panda, penye kichwa cha njia hizo mbili, ili atumie uganga; alititikisa mishale huko na huko, akiziuliza terafi, akayatazama maini” (Ezekiel 21:21). Kwa hiyo miguu na ardhi vina nafasi kubwa sana katika ulimwengu wa roho. Omba sana juu ya maeneo hayo mawili ili Mungu akuongoze njia na mapito yako. Karibia nusu ya ndoto ambazo wapendwa wamekuwa wakinitumia zinahusu ardhi na miguu na uhusiano katika maamuzi ambayo watu wanatakiwa kuyafanya au wameyafanya. Wakati mwingine Mungu anasema nao eneo walilokwama ambalo wanatakiwa wavuke.
Ulimwengu wa roho ni mpana sana na kuna mengi ambayo hatuelewi. Neno linasema watu wanaangimizwa kwa kukosa maarifa (Hosea 4:6). Ila moja ya maombi ambayo yamekuwa yakinisaidia ni maombi ya miguu. Hii imenipa kuwa nasikia zaidi mpango wa Mungu katika maisha yangu na kile Mungu anataka nifanye kwa wakati aliuokusudia.
Katika maombi yetu weekend hii tutaenda kuomba zaidi kuombea miguu sawasawa na neno la Mungu linavyosema kusudi Mungu aweze kusema nasi juu ya mpango wake. Kuna maombi ambayo yanaleta uponyaji wa ardhi/nchi (2 Nyakati 7:14).
Ni imani yangu kwamba katika mwaka 2017 utaweza kumsikia Mungu ataposema nawe juu ya mpango wake katika maisha yako. Nakuombea wewe unayesoma hili somo kiu yako wakati wote iwe kuyatenda mapenzi ya Mungu. Mungu akufunulie akili zako uyaelewe maandiko (Luka 24:45) ili kipaumbele chako kiwe kuutafuta ufalme na haki ya Mungu kwanza (Matayo 6:33).

No comments:

Post a Comment